HIVI karibuni, niliandika mada “mahaba niue ni matokeo ya kuokosea vipimo vya mapenzi.” Huo ndiyo ukweli na makala haya ni maarifa kwako ili upate namna bora ya kuujua mzani wa mapenzi, kupima na kujua kutengeneza ulinganifu (kubalansi).
Huko nyuma, nimewahi kuandika mada inayosema, “Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi”. Nilieleza kwa upana jinsi ya kukabili. Leo nimekuja na muongozo wa jinsi ya kufanya ili uyaweze mapenzi na kuushinda ugumu uliopo.
Mada hii siyo tu lengo lake ni kukufanya ujue mzani, kuyapima mapenzi na kubalansi, pia itakufanya uyaelewe mapenzi. Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.
Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huohuo ukawa unajali za kwako. Kwa pamoja ndipo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote.
Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote. Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.
Penda kuamini kuwa “hili nalo litapita” kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.
Ukitaka kulazimisha awe mchangamfu kwako kipindi ambacho amenuna, ni sawa na kukaribisha matatizo zaidi. Ni vyema kuelewana, watu wengi wanakosea katika uhusiano wao kwa sababu hawatumii busara ili kuwaelewa wenzi wao pindi wanapoonesha hali tofauti.
Busara iendelee kuchukua nafasi. Maneno “hili nalo litapita” liwe somo kwako. Kwamba leo umerudi nyumbani, umetaka chakula cha faragha, mwenzako amekwambia hajisikii vizuri. Hutakiwi kupandisha mizuka na kusababisha nyumbani pasilalike kwa siku hiyo.
Badala yake unapaswa kuvumilia. Jiulize mmefanya tendo mara ngani katika uhusiano wenu, iweje siku hiyo akwambie hajisikii? Ukilazimisha ni sawa na kumfanyia mwenzako ubakaji. Si ajabu akikuona unakuwa mkali, akakubali kukupa kwa shingo upande lakini si kwa ridhaa yake.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi kwa maana, nyakati nyingine utalazimika kuvumilia mambo ambayo pengine yakakuumiza. Mko wawili na kujenga tafsiri ya mwili mmoja. Pengine hata makundi yenu ya damu ni tofauti. Ilivyo maumbile yenu ni hasi na chanya ndiyo na damu zenu zilivyo.
Tofauti hiyo mnaielewa na kuikubali, iweje siku ukirudi nyumbani unamkuta amenuna na hataki kuzungumza na wewe ushindwe kuelewa? Hapo ndipo uvumilivu wako unahitajika. Ni kipindi ambacho busara zako zinapaswa kufanya kazi kwa asilimia 100. Usilazimishe afanye upendavyo wakati mwili wake haupo tayari.
Unaingia faragha na mwenzi wako. Ameshindwa kukuridhisha kabisa. Ni hekima yako kutambua kwamba siku hazilingani. Mbona siku nyingine alikupa mambo mazuri mpaka ukasema ‘poo’? Tatizo ni nini? Pengine nishati za mwili wake kwa siku hiyo hazipo sawasawa na hata yeye mwenyewe hajui.
Ukimkejeli kuwa hajiwezi ni sawa na kumchinjia baharini. Siku zinazokuja atashindwa kabisa. Si kwa sababu uwezo wake ni mdogo, la hasha!
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
1 comment:
Thats True Brother
Post a Comment