Ikiwa unataka tengenezewa Blog, Tukiko lolote la Harusi,Msiba, Mahafali, Tamasha, Matangazo auHabari yoyote usisite kututumia kupitia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com. Follow me instagram @officialfredynjejeblog Twitter @Fredynjeje
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akihutubia wakaazi wa Kituo cha Makazi ya Wazee na Watu Walemavu cha Nunge, Kigambo ni, jijini Dar es salaam
alikotembelea na kusikiliza mahitaji yao pamoja na kutoa msaada wa
mchele kilo 3000, Unga kilo 3000 na Maharage Kilo 1200 ikiwa msaada wake
kwa wazee na walemavu hao.
HOTUBA YA
MHESHIMIWA MAMA JANETH MAGUFULI, MKE WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KWENYE KITUO CHA MAKAZI YA WAZEE NA WATU WALEMAVU WASIOJIWEZA
NUNGE,
KIGAMBONI, TAREHE 3 FEBRUARI, 2016
Mheshimiwa Bibi Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya
Temeke,
Ndugu Ojuku Mgedzi, Mkuu wa kituo cha Nunge,
Ndugu Viongozi mliopo hapa,
Wananunge wote,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Asalaam aleikhum, Bwana Yesu asifiwe, Tumsifu
Yesu Kristo.
Awali
ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha
mahali hapa leo hii tukiwa salama na afya njema. Aidha, napenda kuushukuru
uongozi mzima wa kituo hiki kwa mapokezi mazuri kwangu mimi binafsi pamoja na
ujumbe nilioambatana nao.
Naombeni
mniruhusu pia kuchukua nafasi hii kuwasilisha kwenu salamu nyingi kutoka kwa Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ameniomba
niwaarifu kuwa yupo pamoja nanyi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali katika kuhakikisha wazee na watu wasiojiweza wanapata huduma
zote muhimu kwa kadri ya uwezo wake.
Wageni
waalikwa,
Mabibi
na Mabwana,
Bila
shaka, sisi sote tuliopo mahali hapa tunatoka kwenye familia au maeneo yenye
wazee au watu wenye ulemavu wasiojiweza. Aidha, sisi sote tunafahamu kuwa wazee
na watu wasiojiweza wanahitaji upendo, kuthaminiwa na kusaidiwa. Mtakubaliana
nami pia kuwa kipimo kimojawapo cha kupima jamii iliyostaarabika na
inayoheshimu misingi ya utu ni kuangalia namna inavyowathamini wazee na watu wasiojiweza.
Jambo
la kutia faraja ni kwamba, nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazothamini na
kuwaheshimu sana wazee na watu wasiojiweza. Miongozo na sera mbalimbali zenye
lengo la kulinda na kutetea maslahi ya
wazee na watu wasiojiweza zimeweza kupitishwa na Serikali, ikiwemo Sera ya
Taifa ya Wazee na Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wa Wenye
Ulemavu. Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 imeeleza pia namna
watu wa makundi maalum, wakiwemo wazee na walemavu, watakavyopewa kipaumbele.
Kwa kuzingatia ilani hiyo, Mheshimiwa Rais katika muundo wa Serikali ameweka
Wizara inayoshughulikia masuala ya walemavu. Uwepo wa kituo hiki cha Nunge na
vituo vingine vingi kama hivi hapa nchini ni kiashiria kuwa nchi yetu
inawaheshimu na kuwathamini sana wazee na watu walemavu wasiojiweza.
Wageni
waalikwa,
Mabibi
na Mabwana,
Nikiri
kwa dhati kabisa mimi nikiwa ni Mke wa Rais, mama, mlezi na mwalimu
nimefarijika sana kuwepo mahali hapa siku ya leo. Uwepo wangu mahali hapa umenipa
fursa ya kubadilishana mawazo na watoa huduma na wahudumiwa kuhusu mafanikio na
changamoto zinazowakabili pamoja na namna ya kuzitatua.
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa uongozi na watumishi wote wa
kituo hiki na vituo vingine nchini kwa kazi kubwa mnayoifanya licha ya kukabiliwa
na changamoto kadhaa. Napenda kuwahakikishia kuwa Watanzania wote tunatambua na
kuthamini sana kujitoa kwenu katika kuwahudumia wazee na watu wasiojiweza.
Changamoto
zenu nimezisikia na nawaahidi kuwa tutashirikiana na wadau wote kuzitafutia
majibu yake. Hata hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuziomba na kuzihamasisha taasisi
za Serikali na zisizo za Serikali kushirikiana katika kutatua changamoto
zinazokabili kituo hiki na vingine vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini,
ambavyo nimeambiwa idadi yake ni 17. Baadhi ya chamoto hizo ni pamoja na
uchakavu wa miundombinu; uhaba wa rasilimali fedha na watu, pamoja na maslahi duni
ya watoa huduma; upungufu wa vitendea kazi na huduma za jamii; pamoja na suala
la uvamizi wa eneo la kituo. Nimefarijika
kwamba miongoni mwa wageni waliopo mahali hapa ni viongozi wa Serikali. Hivyo, ni
matumaini yangu kuwa wamechukua changamoto zenu, hususan suala la uvamizi wa
eneo hili la kituo, na kwamba watatafuta ufumbuzi.
Wageni
waalikwa;
Mabibi
na Mabwana,
Ni
dhahiri kuwa Serikali ina wajibu mkubwa katika kuhudumia wazee na watu
wasiojiweza. Hata hivyo, mtakubaliana nami kuwa Serikali pekee haiwezi kumaliza
matatizo yote yanayowakabili wazee na watu wasiojiweza. Hivyo basi, sisi sote kwa
pamoja tunao wajibu wa kusaidia nguvu za Serikali katika kuwahudumia wenzetu
hawa. Na kwa kutambua hilo, mimi na wenzangu nilioambatana nao tumeamua kutoa
zawadi yetu ndogo kwenu. Zawadi hiyo inajumuisha vitu vifuatavyo:
i.
Mchele
kilo 3000
ii.
Unga
kilo 3000
iii.
Maharage
kilo 1200.
Kulingana na idadi yenu
niliyopewa kila mmoja atapewa kilo 25 za
mchele, kilo 25 za unga na kilo 10 za maharage.
Natambua zawadi tuliyoileta ni ndogo
na haiwezi kumaliza matatizo yote mliyonayo. Lakini ni matumaini yangu kuwa
zawadi hii inaweza kuwa chachu ya kuamsha hamasa ya kwa watu na vikundi vingine
kujitoa kusaidia watu wasiojiweza. Ni imani yangu kuwa endapo watu wote
tutajitoa kwa dhati tutaweza kuwahudumia wazee na watu wasiojiweza na hivyo
kuwapunguzia makali ya maisha. Tukakumbuke ya kuwa ‘kutoa ni moyo ni si
utajiri” na kwamba “sisi sote ni wazee na walemavu watarajiwa”.
Mheshimiwa Mkuu wa
Wilaya
Mkuu wa kituo,
Mabibi
na Mabwana,
Napenda
kuhitimisha hotuba yangu fupi, kwa kutoa tena Shukrani zangu za dhati kwa
uongozi wa Kituo kwa kunikaribisha vizuri mimi na wenzangu na pia kwa kazi
kubwa mnayoifanya ya kuwahudumia wenzetu wenye shida mbalimbali.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment