Social Icons

Friday 13 May 2016

Tigo yapinga kuwalipa AY, MwanaFA Sh2 bilioni

Ikiwa unataka tengenezewa Blog, Tukiko lolote la Harusi,Msiba, Mahafali, Tamasha, Matangazo auHabari yoyote usisite kututumia kupitia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com. Follow me instagram @fredynjejeblog Twitter @Fredynjeje


Ambwene Yesaya na Hamisi Mwinjuma 

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya MIC Tanzania (Tigo) imekata rufaa kupinga hukumu iliyoamuru iwalipe Sh2 bilioni wanamuziki wawili, Ambwene Yesaya na Hamisi Mwinjuma kutokana na kutumia bila ya ridhaa yao, nyimbo za wasanii hao nyota nchini.
Yesaya, ambaye ni maarufu kwa jina la kisanii la AY na Mwinjuma anayejulikana kwa jina la MwanaFA, walifungua kesi hiyo ya madai kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala kupinga kitendo cha kampuni hiyo ya huduma za simu kutumia nyimbo zao kwenye miito ya simu bila ya ridhaa yao.
Nyimbo mbili zilizotumika kwenye miito hiyo ya simu ni “Dakika Moja” na “Usije Mjini” ambazo nyota hao wameshirikiana.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Juma Hassan alitoa hukumu ya kesi hiyo Aprili 11, akiwapa ushindi wasanii hao maarufu katika muziki wa vijana uliopachikwa jina la Bongo Fleva.
Katika hukumu hiyo, Mahakama iliiamuru Tigo kulipa Sh5 milioni kama faini ya uharibifu na kulipa Sh2.16 bilioni kama faini ya jumla.
Iwapo wasanii hao watashinda rufani hiyo, watakuwa wameandika historia katika matumizi ya Sheria ya Haki Miliki na watakuwa wasanii wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya kufungua kesi na kushinda.
Katika rufaa hiyo, Tigo kupitia kampuni ya Law Associates imeainisha sababu saba za rufani, ikidai hakimu wa Mahakama ya Ilala alikosea kisheria kuwapa ushindi wasanii hao kwa kuwa hawakuthibitisha madai yao wala hasara waliyopata.
Kampuni hiyo pia inadai kuwa mbali na kutoeleza hasara waliyoipata kutokana na kazi zao kutumika kwenye miito ya simu, walitakiwa kueleza faida ambayo wangepata kama kazi zao zisingetumika kwenye miito hiyo.
Sababu nyingine ya Tigo kukata rufaa hiyo ni wasanii hao hawakuwa wamesajili kazi zao Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota).
Tigo inadai kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, wadai walisema wamesajili kazi hizo, lakini waliwasilisha barua ya Baraza la Sanaa (Basata) ya kutambua kupokea kazi zao na si cheti cha usajili cha Cosota.
Kwa mujibu wa Tigo, wanamuziki hao walipaswa kuwasilisha mahakamani cheti cha usajili wa Cosota ambako kuna utaratibu wa kujisajili ikiwa ni pamoja na kujaza fomu maalumu baada ya kulipia malipo ya usajili ya kila mwaka.
Kampuni hiyo inasisitiza kuwa wasanii hao hawakuwa na haki ya kudai fidia hiyo wakati hawajasajili kazi hizo Cosota na hivyo kuiomba Mahakama Kuu itengue hukumu iliyowapa ushindi.
Akizungumzia hukumu iliyowapa ushindi, MwanaFA alisema huu ni wakati wa mabadiliko.
“Wale waliokuwa wanachukulia Sheria ya Hakimiliki kama mzaha, watambue kwamba zama zimebadilika,” alisema nyota huyo wa muziki wa rap ambaye aliingia kwenye muziki akijitambulisha kama Mwanafalsafa kabla ya kufupisha jina lake na kuwa MwanaFA.
“Hakuna anayetilia maanani kutumia kazi za wasanii bila ridhaa yao huku akinufaika na wasanii kubaki wanalialia. Huu ni wakati wa kutambua kuwa inawezekana kupata haki yako iwapo utasimama kidete kuitetea kwa sababu sheria zipo.”
Akisisitiza, AY ambaye pia ni nyota katika muziki wa rap aliyeimba R&B akishirikiana na Diamond katika siku za karibuni, alisema huo ni mwanzo wa wasanii kufunguka masikio na kutambua haki zao.
Alisema wasanii wamekuwa wakilalamika juu ya haki za kazi zao, lakini hawachukui hatua.
“Wakati ni sasa, muziki ni kazi kama kazi nyingine na ni ajira pia, hivyo unastahili kuheshimiwa,” alisema AY.

No comments: