Social Icons

Friday 20 October 2017

MAMA SHUJAA WA CHAKULA WAPAZA SAUTI KIMATAIFA


Mratibu wa kampeni ya kuwezesha wanawake kutoka Oxfam Bi.Magdalena Thomas akielezea kwa ufupi hali ilivyo katika suala zima la kuwawezesha wanawake linavyohitaji nguvu zaidi huku akitolea mfano namna Mama Shujaa wa Chakula ilivyofanikiwa kuleta mtazamo chanya na kufumbua macho washiriki pamoja na jamii inayowazunguka.


Sambamba na hilo aligusia safari iliyowahusisha washindi wawili wa Mama Shujaa wa Chakula Bi. Elinuru Pallangyo mshindi wa mwaka 2014 pamoja na Bi.Maria Mbuya mshindi wa mwaka 2016 ambao walizuru nchi za Uholanzi pamoja na Italia na kukutana na wabunge nchini humo.
Mshindi wa Mama Shujaa wa Chakula 2014 Bi. Elinuru Pallangyo akielezea namna safari hii ilivyompa fursa ya kupaza sauti Kimataifa kueleza uhalisia uliopo katika jamii ya Tanzania hasa katika sekta nzima ya kilimo na namna wakulima wadogo hususan wanawake wanavyohitaji kushikwa mkono ili kuboresha uzalishaji pamoja na kukuza kipato.

"Miongoni mwa mambo niliyopazia sauti ni kuwahamasisha wenzetu walioendelea kupitia mashirika pamoja na serikali kuja kuwekeza zaidi wakitulenga wakulima wadogo wanawake kwani mchango wetu ni mkubwa lakini mazingira siyo rafiki sana kuweza kutimiza malengo"  alisema Bi.Elinuru.

Akizungumza katika mkutano huo Mshindi wa Mama Shujaa wa Chakula mwaka 2016 alisema yeye alijikita katika kuelezea changamoto zinazowakabili wanawake katika uendeshaji wa kilimo nchini huku akianisha kuwa suala la umiliki wa ardhi, wataalamu wa kilimo, miundombinu pamoja na mabadiliko ya tabia nchi vimekuwa vikwazo vikubwa kwani wengi wakulima wadogo hasa wanawake ni wenye mitaji midogo.


Naye Mratibu wa Kampeni ya chakula na mabadiliko ya tabia nchi kutoka Oxfam Bi. Nuria Mshare amesema  Oxfam ni shirika la kimataifa linalofanya kazi katika nchi 90,ikiwemo Tanzania,ambapo lengo moja wapo ni kufanikisha mabadiliko endelevu kwa kuwainua wakulima wanawake wadogo kwa kuwasaidia katika sekta ya kilimo.

Sambamba na hilo aliongeza kuwa miongoni mwa juhudi zinazofanywa na Oxfam ni kushawishi serikali kuongeza bajeti katika wizara ya kilimo na pia kuezidi kushawishi wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta ya kilimo na hasa kwa wakulima wadogo.

Na Dickson Mulashani

No comments: